Featured
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo KITAIFA. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo KITAIFA. Onyesha machapisho yote

Jumapili, 26 Juni 2016

Breaking News: Orodha Ya Majina Ya Wanafunzi Waliochaguliwa Kujiunga Na Kidato Cha Tano Na Vyuo Vya Ufundi Kwa Mwaka 2016


OR-TAMISEMI inawatangazia majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi kwa mwaka 2016. 

Wanafunzi waliochaguliwa ni kutoka shule za Serikali na zisizo za Serikali. Jumla ya wanafunzi 65,720 wakiwemo wasichana 29,457 na wavulana 36,263 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi. 

Kati ya wanafunzi waliochaguliwa 34,064 wakiwemo wasichana 13,466 na wavulana 20,598 sawa na asilimia 52 watajiunga na masomo ya Sayansi na Hisabati; na wanafunzi 30,897 wakiwemo wasichana 15,445 na wavulana 15,452 sawa na asilimia 47 wamechaguliwa kusoma masomo ya Sanaa na Biashara na wanafunzi 759 wakiwemo wasichana 220 na wavulana 539 sawa na asilimia 1 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya Ufundi.

Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano mwaka 2016 wataanza muhula wa kwanza tarehe 11 Julai, 2016 na hakutakuwa na mabadiliko yoyote ya shule. 


Wanafunzi wote wanatakiwa kuripoti katika shule walizopangwa kwa wakati. Endapo mwanafunzi atachelewa kuripoti hadi tarehe 24 ambayo ndiyo siku ya mwisho ya kuripoti, nafasi yake itachukuliwa na mwanafunzi mwingine aliyekosa nafasi.

Imetolewa na Katibu Mkuu,
OR-TAMISEMI


Tumia link hii kupata matokeo Waliochaguliwa kidato cha tano na vyuo vya ufundi 2016

Jumanne, 3 Mei 2016

Afungwa kwa kuajili wafanyakazi wa darasa la saba



MKUU wa Chuo cha Uhasibu (IAA) Njiro mkoani Arusha, Profesa Johannes Monyo amehukumiwa kifungo cha nje kwa sharti la kutofanya kosa lolote ndani ya mwaka mmoja.

Hukumu hiyo ilitolewa Ijumaa iliyopita na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Devotha Msofe baada ya kujiridhisha kuwa Profesa Monyo alifanya makosa ya kuajiri watumishi wanane wenye elimu ya darasa la saba bila kufuata misingi na kanuni za utumishi wa umma.

Hakimu Msofe alisema Profesa Monyo akiwa Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Njiro, aliwaingiza watumishi wanane kwenye ajira ya kudumu bila ya kibali kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi au Katibu Mkuu Utumishi.

Alisema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani kwa mashahidi 10 pamoja na vielelezo vinane vilivyotolewa mahakamani hapo na upande wa mshtakiwa kuwa na mashahidi wawili, mahakama hiyo imejiridhisha pasipo shaka kuwa Profesa Monyo alifanya kosa hilo la kuajiri wafanyakazi hao wanane bila kufuata taratibu za kisheria.

“Mahakama imejiridhisha pasipo shaka kuwa ulifanya kosa hili la kuajiri wafanyakazi wanane bila kufuata misingi na kanuni za utumishi wa umma hivyo mahakama hii inakutia hatiani kwa kukupa kifungo cha nje kwa sharti la kuutofanya kosa lolote katika kipindi cha mwaka mmoja,”alisema Hakimu Msofe.

Awali, Mwanasheria kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Adam Kilongozi alidai kuwa Juni, 2010 Profesa Monyo anatuhumiwa kuwapa ajira watumishi wanane ambao ni Pamela Maboko, Samson Mbarya, Mawazo Ndaro, Juma Nyarutu, Lilian Ngowi, Godfrey Mollel, Musa Maiki na Salim Shabani.

Kosa jingine ni Profesa Monyo kwa kutumia mamlaka yake vibaya,kuwaingiza watumishi hao wanane katika ajira, ilhali akijua elimu zao ni darasa la saba. Hata hivyo, baada ya hukumu hiyo kutolewa, Profesa Monyo ameonesha kusudio la kukata rufaa kupitia kwa wakili wake, Severine Lawena.

Baada ya hukumu hiyo kutolewa, mwandishi  alimhoji Mwanasheria wa Takukuru, Kilongozi, kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma au Kanuni zake inasemaje juu ya mtumishi anapohukumiwa akiwa bado yupo kazini, ambapo alisema kama mtuhumiwa amehukumiwa na akaonesha nia ya kukata rufaa, basi hukumu hiyo inaweza kufanya kazi au kutofanya kazi hadi hapo rufaa itakaposikilizwa.

Alisisitiza kuwa Takukuru wameshatuma nakala hiyo ya hukumu Tume ya Utumishi wa Umma, mwajiri wa Profesa Monyo, ili mamlaka husika zilifanyie kazi suala hilo lakini pia ni lazima mwajiri wake naye ajiridhishe na hukumu hiyo.

Wafanyakazi wa Kiwanda cha Urafiki na Kampuni ya Vinywaji ya Pepsi (SBC) Wagoma.......Mabomu Yatumika Kuwatuliza, Polisi Apigwa Jiwe Kichwani



Miezi michache baada ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kukwaruzana na Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea chanzo kikiwa ni mgogoro wa Kiwanda cha Urafiki na kupelekana mahakamani, jana mabomu yalirindima kiwandani hapo wakati wafanyakazi wakiendeleza madai ya malimbikizo ya mishahara. 

Awali, viongozi hao walifikishana mahakamani baada ya Kubenea kudaiwa kumtukana Makonda ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati wakitatua moja ya migomo ya wafanyakazi hao. 

Kubenea alihukumiwa kifungo cha miezi mitatu nje na kutotakiwa kutoa lugha ya matusi kama alivyofanya kwa mkuu huyo, lakini madai ya wafanyakazi wa Urafiki bado hayajapata suluhu. 

Katika vurugu hizo zilizoanza jana asubuhi askari mmoja alipigwa jiwe kichwani huku wafanyakazi watatu wakizirai. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime alisema vurugu hizo zilianza baada ya wafanyakazi hao kutoelewana. 

“Waliokuwa tayari kuendelea na kazi walizuiwa na wenzao,” alisema Fuime. 

Akizungumzia kuhusu askari kupigwa jiwe baada ya kuwasili eneo la tukio huku wafanyakazi watatu wakizirai alisema: “Wamepelekwa hospitali na tunawashikilia watu wanne.”

Mgomo huo ulianza mwishoni mwa mwaka jana wakati wafanyakazi hao wakidai stahiki ya mishahara na posho za usafiri, chakula na pango la nyumba. 

Hukumu ya madai iliyotolewa Februari mwaka jana na Mahakama ya Kazi (CMA) iliagiza wafanyakazi hao zaidi ya 800 walipwe Sh4.5 bilioni kuanzia Aprili 30. 

Jana wakati wakifuatilia utekelezaji wa hukumu hiyo, vurugu zilitokea huku magari zaidi ya 10 yaliyosheheni askari yakiwasili eneo la kiwanda hicho na kufanikiwa kutuliza vurugu hizo. 

Meneja Rasilimali Watu wa kiwanda hicho, Dickson Machilika alisema uongozi upo tayari kuwalipa stahiki zao, lakini umepanga kulipa kwa awamu. 

Alisema uzalishaji wa kiwanda umeshuka na hata wafanyakazi wanaingia mara moja tofauti na awali kulipokuwa na awamu tatu. 

Wakati huohuo, Wafanyakazi wa Kampuni ya Vinywaji ya Pepsi (SBC) jana waligoma wakishinikiza uongozi wao kuwapa mikataba ya kuongezewa mishahara. 

Katika mgomo huo, polisi walilazimika kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya wafanyakazi hao ambao walikuwa mbele ya lango la kampuni hiyo wakiimba. 

Wafanyakazi hao waliilaumu kampuni hiyo kwa kumpa wakala jukumu la kuajiri na kulipa mishahara yao jambo linalosababisha ucheleweshwaji wa malipo. 

“Wakala hatumtaki na kwa nini kampuni kubwa kama hii badala ya kuajiri watu, wanawapa mawakala na kusababisha sisi kutolipwa haki zetu,” alisema Dunia Shabani.

Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Irenus Mushongi alisema anashangaa kitendo hicho kwani walifanya mazungumzo na wafanyakazi hao na walikuwa katika hatua za kutafuta ufumbuzi.

 “Mipangilio ipo tena kwa mujibu wa sheria nashangaa kabla ya makubaliano wamelianzisha,” alisema. 

Ofisa Kazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi na Ajira, Omari Sama alisema madai hayo yalifikishwa wizarani na kujadiliana na pande zote na kutoa muda kwa mwajiri kutekeleza madai yao ndani ya siku 30.

Mlinzi wa Wizara ya Ujenzi atupwa jela miaka mitatu Kwa Kosa la Kushindwa Kuzuia Wizi wa Kiti na Kompyuta


Mkazi wa Temeke Ramadhani Kusena (48) amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya kushindwa kuzuia wizi usitokee katika Wizara ya Ujenzi, wakati akiwa mlinzi wa eneo hilo. 

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Catherine Kioja alisema jana kuwa mahakama imemtia hatiani mshtakiwa huyo baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wanne. 

Mbali na kifungo hicho, mahakama pia imemuamuru mshtakiwa huyo kulipa fidia ya Sh500,000 kwa kushindwa kuzuia wizi wa kiti na kompyuta katika chumba namba 303 kilichopo katika ofisi za wizara hiyo. 

Hakimu Kioja alisema mshtakiwa huyo anaweza kukata rufaa kama ataona hajatendewa haki na mahakama hiyo katika hukumu hiyo. 

Awali, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Grace Mwanga uliomba mahakama kutoa adhabu kulingana na shtaka hilo. Hata hivyo, Mahakama ilimpa nafasi mshtakiwa ajitete kwanini asipewe adhabu. 

Akijitetea, mshtakiwa huyo aliomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa anategemewa na familia. Wakili Mwanga alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo Julai 7, 2014 katika ofisi za wizara hiyo Mtaa wa Samora Dar es Salaam.
Copyright © 2015 TANZANIA YETU
| Distributed By Gooyaabi Templates